Jumatano, Januari 31, 2024

MZIZE APIGA TATU YANGA YASHINDA 5-1 ASFC

 

MZIZE APIGA TATU YANGA YASHINDA 5-1 ASFC


KIKOSI cha Yanga leo kimefanikiwa kutinga Raundi ya Tatu ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federatión Cup (ASFC) kufuatia ushindi wa 5-1 dhidi ya Hausung ya Njombe Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga leo yamefungwa na kiungo, Jonás Mkude dakika ya 20, winga Mahalatse ‘Skudu’ Makudubela dakika ya 25 na mshambuliaji Clement Mzize, matatu dakika za 27,33 na 57, wakati bao pekee la Hausung limefungwa na Tonny Jailos dakika ya 70.
Mechi nyingine za Azam Sports Federatión Cup leo Mtibwa Sugar imeichapa Nyakagwe mabao 3-0 Uwanja wa Manungu Complex, Turiani mkoani Morogoro na Kagera Sugar imeilaza Dar City 4-0 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Raundi ya Pili ya ASFC itakamilishwa kesho kwa mchezo kati ya Simba SC na Tembo FC ya Tabora Uwanja wa Azam Complex.

BAFANA BAFANA YAITUPA NJE MOROCCO, MALI YAING’OA BURKINA FASO

 

BAFANA BAFANA YAITUPA NJE MOROCCO, MALI YAING’OA BURKINA FASO


TIMU ya Afrika Kusini imefanikiwa kutinga Robo Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Morocco usiku wa kuamkia leo Uwanja wa Laurent Pokou mjini San-Pedro nchini Ivory Coast.
Mabao ya Bafana Bafana yalifungwa na Evidence Makgopa dakika ya 57 na Teboho Mokoena dakika ya 90 na ushei.
Haikuwa siku kabisa kwa Simba wa Atlasi, kwani mbali na Achraf Hakimi kugongesha kwenye nguzo mkwaju wa penalti dakika ya 83 uliotolewa na Refa Mahmood Ismail wa Sudan baada ya Teboho Mokoena kuunawa mpira, lakini Sofyan Amrabat alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Mokoena dakika ya 90 na ushei.
Bafana Bafana itakutana na Cape Verde Jumamosi ya Februari 3 Uwanja wa Charles Konan Banny mjini Yamoussoukro katika Robo Fainali.


Katika mchezo uliotangulia wa Hatua ya 16 Bora jana, Mali iliitupa nje Burkina kwa kuichapa mabao 2-1 Uwanja wa Amadou Gon Coulibaly mjini Korhogo.
Mabao ya Mali yalifungwa na Edmond Tabsoba aliyejifunga dakika ya tatu na Lassine Sinayoko dakika ya 47, huku la Burkina Faso likifungwa na Nahodha wake, Bertrand Traore dakika ya 57.
Mali itakutana na wenyeji, Ivory Coast katika Robo Fanali Jumamosi.
Robo Fainali nyingine ni Nigeria na Angola na DRC dhidi ya Guinea Ijumaa ya Februari 2.